8 Mei 2021 - 13:08
WHO yaidhinisha chanjo ya COVID-19 ya China

Shirika la Afya Duniani, WHO limeorodhesha chanjo ya Sinopharm kwa matumizi ya dharura dhidi ya COVID-19, na kuiruhusu isambazwe ulimwenguni.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Chanjo ya Sinopharm inayozalishwa na Beijing Bio-Institute of Biological Products Co Ltd, kampuni tanzu ya China National Biotec Group CNBG, zote za nchini China, inakuja baada ya chanjo nyingine kama Astrazeneca Oxford, Johnson & Johnson, Moderna, Pfizer-BioNTech kuwa tayari zimeidhinishwa na WHO. 

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa upatikanaji wa vifaa tiba wa WHO, Dkt  Mariângela Simão alisema Ijumaa kuwa, "kuongezwa kwa chanjo hii kuna uwezo wa kuharakisha upatikanaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi zinazotaka kulinda wafanyakazi wa afya na watu walio katika hatari. Tunamsihi mtengenezaji kushiriki katika mfumo wa COVAX na kuchangia lengo la usambazaji wa chanjo ulio na usawa." 

Utaratibu wa WHO Kuorodhesha Matumizi ya Dharura, EUL, ni sharti la usambazaji wa chanjo la COVAX. Pia unaruhusu nchi kuharakisha idhini yao ya kisheria ya kuagiza na kusimamia chanjo za COVID-19. 

Kwa msingi wa ushahidi wote unaopatikana, WHO inapendekeza chanjo hii kwa watu wazima wenye umri wa miaka 18 na zaidi, kwa utaratibu wa dozi mbili, ambapo dozi ya kwanza na ya pili zinaweza kutenganishwa kwa wiki tatu hadi nne. Ufanisi wa chanjo hii umekadiriwa kuwa asilimia 79, makundi yote ya umri yakiwa yameunganishwa.  

342/